DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Aliyofanyiwa mwalimu Batuli huko Arusha ni Unyama.
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
UKATILI WA KUTISHA ARUSHA: MKURUGENZI WA JIJI NA MBUNGE VITI MAALUM WATAJWA KWENYE JARIBIO LA KUUA. Mwalimu Batuli Hamad (pichani kushoto) ...

UKATILI WA KUTISHA ARUSHA: MKURUGENZI WA JIJI NA MBUNGE VITI MAALUM WATAJWA KWENYE JARIBIO LA KUUA.

Mwalimu Batuli Hamad (pichani kushoto) ametekwa, kupigwa, kutobolewa tumboni kwa kitu chenye ncha kali, na kuchomwa sindano inayodhaniwa ni ya sumu kisha kutelekezwa porini bila fahamu huko mkoani Arusha usiku wa jumatatu tarehe 03/10/2016, katika tukio linalodhaniwa kuratibiwa na Mkurugenzi wa jiji la Arusha Ndg.Athumani Kihamia na Mbunge wa viti maalumu mkoani humo (CCM) Catherine Magige.

Mwalimu huyo wa shule ya msingi Unga Ltd Arusha anahusisha tukio la kutekwa kwake na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mgogoro uliopo baina yake na Mkurugenzi wa jiji hilo na mbunge huyo wa viti maalumu.

Tukio hilo limeripotiwa kituo cha polisi kati Arusha na kupewa RB namba AR/RB/12730/2016.

#Matukio_Kabla_ya_Kutekwa

Tarehe 17/08/2016 Mkurugenzi wa jiji hilo Ndg.Athumani Kihamia alimpandisha cheo Mwalimu Batuli kuwa Mratibu wa Elimu kata ya Ngarenaro. Uteuzi huu ulitokana na Mwalimu huyo kukidhi vigezo vyote muhimu vya kitaaluma na uzoefu kazini. Batuli ana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika tasnia ya ualimu, na shahada ya elimu baada ya kujiendeleza kimasomo. Kwahiyo uteuzi wake kuwa mratibu elimu kata ni jambo ambalo alistahili.

Mwalimu huyu anadai kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika nafasi yake mpya. Lakini ghafla tar.19/09/2016 mwezi mmoja tu baada ya kuteuliwa, aliandikiwa barua na Mkurugenzi Kihamia ya kutengua uteuzi wake wa Mratibu wa Elimu na kumrudisha shule ya Msingi Unga Ltd akaendelee kufundisha.

Lakini barua ya Mkurugenzi Kihamia haikueleza kwanini amemshusha cheo Mwalimu Batuli. Barua hiyo ilisema tu kwamba Batuli ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya Mratibu elimu lakini haikusema ni majukumu gani ambayo Batuli alishindwa kutimiza.

Mwalimu Batuli hakuridhika na maamuzi hayo, kwa sababu hakuelezwa kosa lake, wala hakupewa nafasi ya kujitetea. Hata hivyo mwezi mmoja tu aliofanya kazi ni kipindi kifupi sana kuweza kupima utendaji wake. Kipindi hiki alitakiwa kufanyiwa "mentorship" na "orientation" ya nafasi yake mpya kabla ya kuanza kupima utendaji wake.

Vilevile Kanuni za utumishi wa umma na sheria ya ajira na mahusiano kazini no.6 ya mwaka 2004, kwa pamoja vinaeleza hatua za kuchukua kwa mtumishi aliyeshindwa kutimiza wajibu wake. Mojawapo ni barua mbili za onyo na nafasi ya kujitetea kabla hajavuliwa madaraka. Lakini haikua hivyo kwa Batuli. Yeye hakuandikiwa hata barua moja ya onyo wala hakupewa nafasi ya kujitetea. Ni dhahiri kuwa hakutendewa haki.

Kwahiyo akatafuta nafasi ya kukutana na Mkurugenzi Kihamia ili ajue sababu ya kushushwa cheo na ajue ni wapi alipokosea ili aweze kufanyia kazi mapungufu yake. Lakini Kihamia alimpuuza na hakumpa nafasi ya kumsikiliza.

Hivyo basi Mwalimu Batuli akaamua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ili kueleza suala lske. Mkuu huyo wa wilaya Ndg.Gabriel Fabian Dagarro alimpokea Mwalimu Batuli na kumsikiliza, ambapo alionesha kushangazwa na uonevu aliofanyiwa. Mkuu huyo wa wilaya aliahidi kufanyia kazi suala hilo kwa kuwasiliana na Mkurugenzi Kihamia.

Mkurugenzi Kihamia hakufurahishwa na kitendo cha Mwalimu Batuli kufikisha suala lake kwa Mkuu wa wilaya kwani alitafsiri kuwa ameenda kushtakiwa. Baada ya hapo ndipo akatekwa na kufanyiwa ukatili wa kutisha.

Mwalimu huyu kwa sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya Mt.Meru. Akiongea na waandishi wa habari amehusisha tukio la kutekwa kwake na mgogoro baina yake na Mkurugenzi Kihamia kwa sababu watekaji wakati wanampiga walikua wakimwambia "Utajutia uamuzi wako wa kwenda kumshtaki Mkurugenzi huko ulikoenda"

Baada ya kuokotwa akiwa amepoteza fahamu Mwalimu Batuli alikimbizwa hospitali ya mkoa ya Mt.Meru ambapo alipewa matibabu na kutibiwa jeraha la tumboni alilotobolewa na kitu kinachodaiwa chenye ncha kali. Hata hivyo haijajulikana sindano aliyochomwa ilikua na kitu gani kingine japo uchunguzi wa awali umeonesha kuwa ilikua na "Insulin"

#Catherine_Magige_anahusikaje?

Kwa mujibu wa Mwalimu Batuli, anasema siku chache baada ya kuteuliwa kuwa Mratibu wa elimu kata ya Ngarenaro aliingia kwenye mgogoro na mbunge Magige kupitia group moja la whatsapp ambalo wote wawili wapo. Katika group hilo Batuli anadai alimkosoa Mbunge Magige ktk mambo mbalimbali yanayohusu ubunge wake. Lakini ukosoaji wake ulikua wa nia njema ili Magige aweze kufanyia kazi mapungufu yake na kuboresha utumishi wake.

Lakini Magige alichukulia ukosoaji huo "in negative perception" na akadhamiria kumchukulia hatua Mwalimu Batuli. Kupitia group hilo la Whatsapp Magige anadaiwa kumwambia Batuli kuwa ATAMSHUGHULIKIA. Na baada ya muda mfupi Mwalimu Batuli akaandikiwa barua ya kutenguliwa katika nafasi yake ya Mratibu wa elimu kata ya Ngarenaro.

Kwahiyo Batuli anaamini alifukuzwa kazi kwa majungu na sio kweli kwamba alishindwa kutimiza wajibu wake wa kazi. Inaaminika kuwa Magige alipeleka majungu kwa Mkurugenzi Kihamia baada ya kukasirishwa na kukosolewa kwenye group la Whatsapp. Kihamia nae akafanyia kazi majungu ya Mbunge huyo na kuamua kutengua uteuzi wa Batuli.

Ndio maana kwenye barua ya kumvua madaraka alishindwa kueleza ni majukumu gani ambayo Batuli alishindwa kutimiza. Na hata Batuli alipoomba kukutana na Mkurugenzi huyo alikataa kwa sababu alijua kwamba amemvua madaraka kwa majungu tu na hakuwa na sababu yoyote ya msingi.

Hii ina maana kuwa mgogoro kati ya Batuli na Magige ulioanzia group la Whatsapp, ulitengeneza mgogoro mpya kati ya Mkurugenzi Kihamia na Batuli, ambao umepelekea yeye kutekwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili.

#MyTake:

1. Rais Magufuli atengue uteuzi wa Kihamia mara moja. Katika kipindi cha miezi miwili tu tangu ateuliwe kuwa mkurugenzi Arusha amegubikwa na kashfa nyingi kuliko wakurugenzi wote nchini.

Wiki jana alipata kashfa ya ufisadi wa mafuta ya gari yake ambapo alitumia lita 1900 badala ya lita 300 alizopewa kwenye bajeti. Sasa ameingia katika kashfa nyingine ya kuhusika kutekwa kwa Mwalimu Batuli. Hivi mtu wa aina hii anaendelea kuachwa madarakani ili iweje? Mnataka afanye makubwa zaidi ya haya ndo mchukue hatua?

Kutekwa kwa Mwalimu Batuli, kupigwa, kuchomwa bisibisi tumboni, na kuchomwa sindano ya "sumu" ni ushahidi kwamba alikusudiwa kuuawa. Yani watekaji waliamini wamemuua Batuli lakini akapona kwa miujiza ya Mungu. Sasa jiulize mtumishi wa umma anayetajwa kwamba alihusika kwenye njama hizi je anastahili kuendelea kubaki kwenye nafasi yake?

2. Mbunge Magige achunguzwe kama kweli alihusika achukuliwe hatua za kinidhamu na chama chake.

3. Waalimu wamekuwa kama yatima nchi hii. Wananyanyaswa, wanaonewa, wanadhalilishwa lakini hawawezi kusema na hata wakisema wanapuuzwa. Sasa ni wakati wa kujitokeza na kupinga uonevu huu.

Kwahiyo nategemea kuona waalimu nchi nzima bila kujali itikadi zao, wakijitokeza na kulaani tukio hili. Nategemea pia wanaharakati wa haki za binadanu na wanaharakati wa masuala ya kijinsia wakijitokeza kwa wingi kulaani ukatili huu dhili ya Mwalimu Batuli. Kwa nguvu ileile mliyojitokeza kulalamikia tukio la Mbeya, mjitokeze kulalamikia tukio hili pia.

Kataa uonevu. Pinga ukatili wa kijinsia. Kataa unyanyasaji katika vituo vya kazi. Pinga viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kunyanyasa wanyonge. #Justice_Batuli.!

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top