Uzinduzi Mradi wa “Ardhi Clinic” na Manufaa yake kwa Taifa
Ndugu Wanahabari;
Awali ya yote, nawashukuru sana kwa kuitikia wito wetu. Leo shirika lisilo la kiserikali la Universal Development Initiative (UDI) – kwa kushirikiana na kampuni ya upangaji na uendelezaji makazi – Human Settlement Action (HUSEA) – tunaomba kupitia kwenu, kuutambulisha rasmi kwa umma wa Watanzania mradi mpya uitwao “Ardhi Clinic”.
Ardhi Clinic ni mradi unaokusudia kujenga uelewa na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa wingi na kwa kasi katika kurasimisha umiliki wa ardhi zao. Mkakati mkuu wa mradi huu ni kuwawezesha wananchi kupima viwanja na mashamba yao kwa gharama nafuu na hivyo kurahisisha upatikanaji wa hati, kupunguza dhuluma, migogoro ya ardhi na kuifanya ardhi kuwa mtaji na dhamana rasmi zaidi katika kuvutia mikopo na fursa mbalimbali za kimaendeleo.
Yapo masuala kadhaa yaliyoisukuma UDI na HUSEA katika kuuandaa mradi huu:
Kwanza, mradi huu ni sehemu ya jitihada za kutekeleza kwa vitendo fikra na dhamira kuu ya shirika la UDI na kampuni ya HUSEA. Siku zote dira kuu ya UDI imekuwa ni “kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu ya jamii ulimwenguni kote, kwa kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali inayochochea utawala bora na uwajibikaji na kuongeza ushiriki na uwezeshaji wa wananchi katika kufanya maamuzi, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo yao”. Dira kuu ya HUSEA ni “kujenga ufahamu juu ya masuala ya ardhi kwa jamii za Tanzania kupitia mijadala mbalimbali na kufanya upangaji na uendelezaji makazi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Pili, tumeguswa na dhamira iliyoonyeshwa na serikali. Mradi unakuja katika wakati ambapo serikali ya awamu ya tano, chini ya Mhe Rais John Pombe Magufuli, imetangaza azima ya kuhakikisha ardhi yote nchini iwe imepimwa ifikapo mwaka 2020. Na katika kulifikia lengo hili kubwa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe William Lukuvi, hivi karibuni aliitaka sekta binafsi kuongeza kasi ya upangaji miji na upimaji ardhi kwa kushirikiana na serikali. Kwa hiyo, mradi huu wa Ardhi Clinic unaunga mkono dhamira hii njema ya Mhe. Rais na tunaitikia wito wa moja kwa moja wa Waziri Ardhi
Tatu, tumesukumwa na matokeo ya tafiti mbalimbali na mahitaji halisi ya Watanzania. Nia yetu ni kushughulikia vikwazo ambavyo kwa miaka mingi vimesababisha sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania kubaki bila kupangiliwa, kupimwa wala kuendelezwa vema. Takwimu za Wizara ya Ardhi za mwezi Mei mwaka huu zinathibitisha kuwa zaidi ya asilimia 85 ya ardhi yote nchini haijapimwa. Swali kubwa la kujiuliza ni nini hasa kimesababisha sehemu kubwa ya ardhi ya nchi kubaki hivyo ilivyo kwa muda mrefu?
Katika jitihada za kujibu swali hili, mnamo mwaka 2010 – 2014 Taasisi ya Masomo ya Maendeleo ‘Institute of Development Studies (IDS)’ ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya utafiti chini ya ufadhili wa Shirika la Denmark (DANIDA). Kwa mujibu wa utafiti huo, kuna sababu kuu sita zilizochangia tatizo hili:
Gharama za upimaji kuwa kubwa kuliko uwezo wa kipato wa Watanzania walio wengi. Sababu hii ilionekana kuwa na uzito kwa 29%
Tatizo la rushwa ambalo lilionekana kuwa kikwazo kwa 35%.
Uelewa mdogo wa wananchi juu ya haki za ardhi. Hii ilionekana kuchangia kwa asilimia 9%.
Miundombinu kuwa duni – hii ilionekana kuwa kikwazo kwa 9%.
Uhamaji wa watu toka vijijini kwenda mijini. Hili lilionekana kuwa na uzito kwa 9%
Na umaskini kwa ujumla ambao ulionekana kuwa unachangia kwa 9%.
Kwa hiyo, matokeo ya utafiti huu ni sehemu ya masuala ya msingi yaliyotuongoza katika kutengeneza mradi huu.
Kazi Kuu za Ardhi Clinic:
Kwa kuzingatia vikwazo hivyo na kusudio letu la kuongeza ushiriki wa wananchi na kasi ya upimaji viwanja na mashamba nchini, UDI kwa kushirikiana na HUSEA na wananchi wenyewe wa maeneo husika, tumejipanga vizuri kufanya kazi kuu zifuatazo;
Kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzitambua na kuzilinda haki zao za ardhi na umuhimu wa kupima ardhi kwa pamoja
Kufanikisha upimaji wa ardhi za wananchi kwa pamoja na kwa gharama nafuu pale ambapo wananchi wanaonyesha uhitaji kupitia serikali za mitaa au vijiji vyao. Unafuu wa gharama utakadiriwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na kampuni ya upimaji na viongozi wa serikali za mitaa wa maeneo husika.
Kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wananchi waliopimiwa ardhi wanapata hati zao kwa wakati uliopangwa na kuepusha rushwa na uchelewaji usio wa lazima.
Kuanzisha huduma za bure za kutoa taarifa rasmi kuhusu ardhi na wamiliki wake kwa kuzihifadhi kwenye kompyuta zitakazowekwa kwenye kila ofisi ya mtaa/kijiji kitakachofikiwa na mradi huu – Land Information System Database. Hii itaziwezesha serikali za mitaa na wananchi kubaini kwa urahisi wamiliki halali wa ardhi ndani ya maeneo yao na kuepusha utapeli katika mauziano ya ardhi.
Kutoa mafunzo ya kuimarisha zaidi ufanisi wa viongozi wa serikali za mitaa katika kusimamia mifumo, sheria na kanuni za ardhi ili kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kuepusha migogoro
Katika kazi hizo, UDI itajikita zaidi kwenye majukumu yanayohusu utoaji elimu na kuhamasisha wananchi kurasimisha ardhi zao pamoja na kuimarisha uwezo wa serikali za mitaa katika kusimamia ardhi. HUSEA, kwa kushirikiana kwa karibu na serikali, itahusika na majukumu yanayohusu upangaji, upimaji ardhi na kurahisisha mchakato wa upataji hati. HUSEA ni kampuni iliyosajiliwa na Bodi ya Mipango Miji kwa shughuli za upangaji miji na uendelezaji makazi nchini.
Manufaa ya Ardhi Clinic kwa Taifa
Utekelezaji Mradi wa Ardhi Clinic unatazamiwa kuwa na faida nyingi za kiuchumi na kijamii kwa mtu mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla. Nitaje chache;
Utawahakikishia wananchi utambulisho na usalama wa kisheria wa ardhi wanazomiliki na kuwaepusha na hatari za kubomolewa majengo, kudhulumiwa au kuondolewa kwenye ardhi husika.
Utarahisisha wananchi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa kutumia hati za ardhi kama dhamana kwa maombi ya mikopo na hivyo itachochea ajira za kujiajiri na kujikwamua kimaisha.
Utatanua wigo na kuongeza mapato ya kodi ya ardhi na kodi ya majengo kwa serikali
Utapunguza kesi na migogoro mingi ya ardhi kwa kadri sehemu kubwa ya ardhi itakavyopimwa, kumilikishwa na kusimamiwa vizuri.
Utarahisisha kufunguliwa kwa huduma nyingi muhimu za kijamii kama maeneo ya wazi kwaajili ya bustani, masoko, viwanja vya michezo, barabara, shule na kupitisha umeme na maji
Utaimarisha amani na usalama wa watu kwasababu ya mpangilio mzuri wa makazi na wepesi wa kuwabaini wakazi wa maeneo husika.
Utachangia kuboreka kwa usafi na afya za watu kwasababu ya mpangilio wa makazï
Utaisadia kutengenezwa kwa anuani rasmi za mitaa yenye makazi na maeneo yaliyopimwa.
Utaongeza uzuri wa mandhari ya miji na majiji kama matokeo ya kupangiliwa vyema kwa mitaa, vitongoji, kata, wilaya, mikoa na nchi nzima kwa ujumla.
Imetolewa leo na:
Edward Kinabo
Mkurugenzi Mkazi
Universal Development Initiative (UDI
Post a Comment