SERIKALI imesema pamoja na maboresho na ujenzi wa makazi ya Polisi, inapitia upya posho ya pango kwa askari polisi ili kuwaondolea adha wanayoipata. Hivi sasa askari anapata posho ya asilimia 15 akiwa katika ngazi ya chini na akipanda daraja, kiwango hicho hakiongezwi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM).
Mulugo katika swali la nyongeza alitaka kufahamu serikali ina mpango gani kuboresha makazi ya polisi na nyumba kiasi gani zitajengwa katika wilaya mpya ya Songwe.
Mwigulu akijibu swali hilo alisema serikali itatoa kipaumbele kwa mikoa na wilaya mpya, ikiwamo ya Songwe katika ujenzi wa nyumba za askari Polisi.
Amesema pia, posho ya pango kwa askari itaboreshwa ili ipande zaidi ya asilimia 15 mhusika anapopandishwa mshahara.
Katika swali la msingi, Mulugo alihoji je, ni lini serikali itajenga nyumba za askari polisi katika Wilaya ya Songwe ikizingatiwa kuwa askari wengi wameripoti ndani ya wilaya hiyo mpya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema serikali inatambua tatizo la makazi ya askari polisi katika wilaya mpya ya Songwe na maeneo mengine hususan mikoa mipya.
"Ni nia ya Serikali kutatua tatizo la upungufu wa makazi ya askari polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima.Mkoa wa Songwe ikiwamo wilaya ya Songwe ni sehemu ya mpango huo utakaoanza kutekelezwa baada ya utararibu wa mkopo wa kuwezesha ujenzi huo kukamilika," alisema Masauni.
Post a Comment