DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Kisutu wafuta kesi ya rushwa ya milioni 162/-
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imefuta kesi ya kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mhandisi Mkuu wa Wakala ...

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imefuta kesi ya kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Theophillo Bwakea.

Bwakea aliyedaiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalila ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Wakili wa Serikali, Odesa Olombe alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaomba mahakama ifute kesi hiyo.

Olombe alidai kuwa wanaomba kufuta kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu namba 98 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu kidogo cha 25 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Kutokana na maombi hayo, wakili wa mshitakiwa Rweyongeza Richard, alidai kuwa hana pingamizi na maombi ya upande wa Jamhuri.

Hata hivyo, Hakimu Mwijage alikubaliana na ombi lililotolewa na upande wa jamhuri na kuifuta kesi hiyo. Inadaiwa kwamba kabla ya Bwakea kufanya kazi REA, alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme (Tanesco).

Inaelezwa kuwa sera hiyo ilipoanza kutumika, Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata zabuni. Inadaiwa Februari 12, 2014 katika Benki ya Mkombozi, mshitakiwa akiwa Mhandisi Mkuu wa REA, kwa njia ya rushwa alijipatia Sh milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901 fedha ambazo ni sehemu ya zilizokuwapo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Pia inadaiwa fedha hizo aliingiziwa katika akaunti yake na Rugemalila ambaye ni mshauri binafsi wa kimataifa, Mkurugenzi wa VIP Engineering na alikuwa Mkurugenzi wa IPTL. Hata hivyo, inadaiwa alipewa fedha hizo kama zawadi kwa kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe walioandaa sera zilizoruhusu sekta binafsi kuuza umeme Tanesco.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top