DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Mtwa Mkwawa. "Mkwavinyika"
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
MSALITI NI ASALI TENDO LAKE NDIYO SHUBIRI Chifu Mkwawa asingejiua bila kusalitiwa. Kama si usaliti wa mtu aliyemwamini, Wajerumani wasingem...

MSALITI NI ASALI TENDO LAKE NDIYO SHUBIRI

Chifu Mkwawa asingejiua bila kusalitiwa. Kama si usaliti wa mtu aliyemwamini, Wajerumani wasingemuweza Mkwawa. Historia nyingi zinaandikwa uongo ili Wazungu waonekane mashujaa wa vita, ila ukweli Mkwawa aliwashinda, lakini baadaye alisalitiwa.

Jina lake ni Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, mtoto wa Chifu Munyigumba. Ukitaka kumzungumzia wala usizunguke sana, sema tu Chifu Mkwawa inatosha.

Kwa nini aliitwa Mkwawa? Hilo linatokana na jina lake “Mkwavinyika” ambalo lilifupishwa na kutamkwa “Mkwava” lakini baadaye watu wakaona ni rahisi zaidi kuita “Mkwawa” kisha ikazoeleka hivyo. Jina mashuhuri kabisa “Chifu Mkwawa.”

Alikuwa na mbinu nyingi za kupigana na kujilinda. Alitengeneza mfumo mzuri wa usalama na alijua jinsi ya kuwakabili Wazungu waliofanya majaribio kadhaa ya kumvamia wakiwa na bunduki pamoja na mizinga. Wajerumani mpaka leo hawawezi kumsahau Mkwawa.

Alikuwa chifu wa himaya ya Wahehe ambayo ndiyo Iringa ya leo na alisambaza mtandao wake wa kichifu kuanzia Kusini mpaka eneo la kati ya Tanzania ya leo, alisalitiwa na mtu aliyemwamini sana, aliyeitwa Mtaki Mwanyenza.

Mtaki hakuwa Mhehe, asili yake ni Mnyamwezi wa Tabora. Alifika Kalenga, yalipokuwa makao makuu ya Serikali ya Chifu Mkwawa, alipowapeleka Waarabu, aliotoka nao Tabora. Waarabu hao walikuwa wanatafuta watumwa,

Mtaki alikuwa mtu mjanja, aliyekuwa na uwezo kujua lugha tofauti na alikuwa anafahamu sifa za himaya ya Chifu Mkwawa, kwamba ina watu wenye nguvu waliowatandika Wajerumani kisawasawa.

Waarabu kwa kuongozwa na Mtaki, walifika mpaka Kalenga, wakakutana na Mkwawa. Katika mazungumzo yao, Mkwawa aliwaambia hawezi kuuza watu. Alisema watu wa himaya yake wote walikuwa sawa, hivyo hakukuwa na mwenye upungufu wa kutosha kuuzwa kama mtumwa.

Baada ya biashara hiyo ya watumwa kutofanyika, walifanya biashara tofauti. Mkwawa aliwauzia Waarabu pembe za ndovu na ngozi za wanyama mbalimbali wa porini kama simba, chui, nyati na kadhalika.

Biashara hiyo ilipofanyika, jambo lingine lilifuata. Mkwawa alipenda ustaarabu wa Waarabu, uvaaji wao hasa ufungaji wa kilemba. Ni hapo Chifu Mkwawa alisilimu kisha akaanza kuvaa kilemba na mavazi mengine aliyoiga kwa Waarabu.

Mkwawa hakuwa mbinafsi, aliwapenda sana watu wake. Zile pembe za ndovu na ngozi za wanyama ambazo aliwauzia Waarabu, walibadilishana na nguo ambazo ziligawanywa kwa watu wa himaya ya Mkwawa. Kihistoria watu wa himaya ya Mkwawa ni miongoni mwa jamii za kwanza Afrika Mashariki kuvaa nguo.

Mtaki alipofanikiwa kuwaunganisha Mkwawa na Waarabu, aliona kuna fursa katika kuwa karibu na Mkwawa. Alianza kwa kumshauri Mkwawa jenge boma la makazi ya chifu ambalo linakuwa limezungushiwa uzio mkubwa wa ukuta. Kabla ya hapo, makazi ya Chifu Mkwawa yalikuwa hayajazungushiwa.

Katika kumjengea hoja, Mtaki alimweleza namna ambavyo maboma mbalimbali ambayo yalikuwa makazi ya watawala wengine yalivyokuwa. Mkwawa alivutiwa na ushauri huo, akakubali kujenga.

Ushauri mwingine kutoka kwa Mtaki kwenda kwa Mkwawa ulikuwa ni kumuoa mtoto wa Mtemi Isike wa Tabora, aliyeitwa Ilagila binti Isike. Mkwawa alipomuoa Ilagila, alimuona Mtaki ni mtu mzuri kwake, akampenda na kumwamini.

Chifu Mkwawa aliamua kumtawaza Mtaki kuwa ni Mhehe na kwa vile Wahehe walikuwa na koo zao, Mkwawa alimtangaza Mtaki kuwa Mhehe wa koo ya Mwanyenza. Ndipo hapo alianza kuitwa Mtaki Myanyenza.

Utaratibu wa vyeo katika utawala wa Mkwawa, alikuwepo chifu mkuu ambaye ndiye Mkwawa, vilevile walikuwepo machifu wasaidizi ambao walifahamika kwa jina la Wanzagila.

Hao Wanzagila walikuwa viongozi wa kanda katika utawala wa Mkwawa. Kulikuwa na kanda nne na kila kanda ilikuwa na Mnzagila (chifu msaidizi). Wanzagila walikuwa wakiripoti kwa Mkwawa. Utaratibu huo ulimfanya Mkwawa atawale kwa urahisi zaidi.

Mkwawa alipomshiba Mtaki, aliamua kumteua naye kuwa Mnzagila lakini hakumpa eneo la kutawala, bali alimfanya kuwa Mnzagila maalum. Jukumu alilompangia lilikuwa usimamizi wa ujenzi wa boma la makazi ya Chifu Mkwawa ambalo liliitwa Lipuli. Ujenzi ulifanyika na kukamilika. Chifu Mkwawa alianza kuishi ndani ya Lipuli.

MKWAWA NA WAJERUMANI

Kabla ya Mtaki na Waarabu kwenda kwa Mkwawa, tayari Wajerumani walikuwa wameshakiona cha mtema kuni kutoka kwa Mkwawa. Hata kipindi Mtaki alipopokelewa na Mkwawa na kuaminiwa, Wajerumani walikuwa wametulia wakitamani ipatikane namna yoyote kuusambaratisha utawala wa Mkwawa.

Historia ipo hivi; mwaka 1885 baada ya kukamilika kwa Mkutano wa Berlin, uliohusu wakuu wa nchi za Ulaya kukutana na kujadiliana jinsi ya kugawana kanda za utawala barani Afrika, Ujerumani ilianza kujitandaza Tanzania Bara (Tanganyika).

Mkutano wa Berlin, ulifanyika kuanzia mwaka 1884 mpaka 1885, Berlin, Ujerumani. Kumalizika kwa mkutano huo, kulisababisha sasa Wazungu kuvamia Afrika. Wajerumani walipowasili Tanzania walianza kueneza ukoloni na kuzifanya tawala mbalimbali za jadi zilizokuwepo zisalimu amri.

Kati ya mwaka 1888 na 1889, Wajerumani walipata wakati mgumu katika Vita ya Abushiri ambayo ilihusu eneo la Pwani ya Tanzania Bara. Ni eneo ambalo pamoja na uwepo wa wenyeji, lilikuwa na Waarabu ambao walikuwa wamelowea. Wenyeji asilia walipambana hasa na Wajerumani.

Mwaka 1889 Wajerumani walifanikiwa kulidhibiti eneo la Pwani ya Tanzania Bara (Tanganyika), baada ya hapo wakaanza kumpigia mahesabu Mkwawa ambaye utawala wake ndiyo ulikuwa bado haujasalimu amri.

Wajerumani walianza maandalizi ya kumvamia Mkwawa. Mwaka 1891 walijipanga kutekeleza oparesheni ya kuubomoa utawala wa Mkwawa. Safari ya Wajerumani kutoka Dar es Salaam kwenda himaya ya Mkwawa, ilianza Julai 1891.

Kikosi cha Ujerumani kiliongozwa na Mkuu wa Majeshi wa Ujerumani-Tanganyika, Emil von Zelewski, kilikuwa na askari takriban 500, Wajerumani wakiwa zaidi ya 40, huku Waafrika waliotekwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na kufanywa askari wa vikosi vya Ujerumani wakiwa zaidi ya 460.

Mkwawa alikuwa na mfumo wa siri wa usalama. Kila kijiji kilikuwa na ofisa usalama ambao waliitwa Watandisi. Wajerumani wapoanza kuingia himaya ya Mkwawa. Mtandisi wa kijiji cha kwanza alikimbia mpaka kijiji cha pili na kumjulisha mtandisi wa eneo hilo kuhusu kuingia kwa Wazungu ambao waliwaita Walangala.

Hivyo, mtandisi wa kijiji cha pili alimfikishia wa kijiji cha tatu, hivyohivyo mpaka mtandisi wa mwisho alipomfikia Mkwawa ambaye alikwenda kwenye ngome yake ya kijeshi,Kalenga, akawaandaa wapiganaji wake.

Watandisi walikuwa watu wenye mbio na walijua njia za mkato, kwa hiyo walifikisha taarifa mapema na jeshi la Mkwawa lilijiandaa kabla ya Wajerumani hawajakaribia makao makuu.

Ni kwamba Wajerumani walimdharau Mkwawa, kwa hiyo hawakujua kama anaweza kuwa na mfumo mkali wa usalama. Walimuona ni kiongozi dhaifu ambaye wapiganaji wake walitumia mikuki na pinde wakati wao walikuwa na bunduki pamoja na mizinga.

Wajerumani walipokuwa njiani walishambulia na kuua watu waliokosa hatia. Walikutana pia na mabalozi watatu wa Mkwawa ambao walitumwa na Chifu Mkwawa ili wazungumze kupata suluhu lakini Zelewski aliagiza wauawe bila kuzungumza nao chochote.

Eneo la pori la Lugalo ndipo Mkwawa na askari wake zaidi ya 300 walijificha kimya. Wajerumani walipovuka Mto Ruaha, walianza kufuatiliwa na walipoingia Lugalo, walijikuta wanavamiwa na kushambuliwa.

Kwa vile walikuwa hawajaandaa bunduki zao, walijikuta wanapigwa kila upande japokuwa walijitahidi kujibu mashambulizi. Wajerumani 40 waliuawa akiwemo bosi wao Zelewski. Baada ya kuwa wamewazidi nguvu, Mkwawa aliagiza Waafrika waliokuwepo kwenye msafara huo wa Ujerumani wasiuawe.

Sababu ni kuwa waliteka bunduki nyingi pamoja na mizinga ambayo wao hawakuwa na utaalamu wa kuitumia. Alitaka Waafrika wabaki hai ili watumike kuwafundisha askari wa jeshi lake jinsi ya kutumia silaha hizo za moto.

Siku ambayo Wajerumani walikomeshwa na Mkwawa Lugalo ni Agosti 17, 1891. Na kwa kumbukumbu hiyo, ikawa sababu ya Kambi ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam, kupewa jina hilo.

Baada ya kuwa na silaha hizo, Mkwawa alianza kuweka utaratibu wa kwenda kushambulia ngome nyingine ambazo zilikuwa zimeshatekwa na Wajerumani ili kujilinda zaidi, hakutaka wawe karibu. Mashambulizi hayo yalizidi kuwatia hasira Wajerumani.

MKWAWA ALIVYOSALITIWA

Baada ya kukamilisha ujenzi wa Lipuli, Mkwawa alimwagiza Mtaki kwenda Dar es Salaam ili akutane na Wajerumani, waeleze mahitaji yao ni nini maana walikuwa wakipigana bila kujua Wajerumani walichohitaji.

Alimteua Mtaki kwa sababu alimuona mjanja-mjanja na kwa vile aliweza kuzungumza na Waarabu, kwa hiyo ilikuwa rahisi kwake kuelewana na Wajerumani. Safari ya Mtaki kwenda Dar es Salaam ikaanza. Huo ulikuwa mwaka 1898.

Mtaki alipofika Dar es Salaam alikutana na Waarabu ambao walimuunganisha na Wajerumani. Mtaki alipojitambulisha kuwa anatoka kwa Mkwawa kwanza hakuminika, aliulizwa maswali mengi na baada ya kuthibitisha walimrubuni.

Wajerumani walimweleza Mtaki kuwa wao wasingeweza kufanya mazungumzo yoyote na Mkwawa kwa sababu aliliaibisha taifa lao hasa kwa akitendo cha kumuua Zelewski. Wajerumani walimshawishi Mtaki akubali kuwapa siri za namna ya kumpindua Mkwawa na baada ya hapo, yeye angefanywa Chifu wa Wahehe.

Ahadi hiyo ya kufanywa Chifu wa Wahehe ilimsisimua Mtaki. Akamwaga siri zote za namna ya kumvamia Mkwawa bila kushtukiwa. Hakuishia hapo, Mtaki aliwaongoza Wajerumani kupitia njia isiyo na ulinzi ya Ifakara, Mgololo, Mufindi mpaka makao makuu ya utawala wa Mkwawa.

Njiani Wanzagila walipomuona Mtaki yupo na Wajerumani wala hawakushtuka, walijua ndiyo alikuwa anawapeleka kwa Mkwawa kwa ajili ya mazungumzo, hawakujua kuwa tayari Mtaki alikuwa ameshauza utawala wao.

Bila kutarajia, Mkwawa alishtuka Kalenga inalipuliwa na mizinga ya Wajerumani. Himaya ya Mkwawa ilidhibitiwa kila upande. Mkwawa baada ya kuona hana namna yoyote na kwa vile alikataa aibu ya kukamatwa na kuteswa na Wajerumani, aliamua kujipiga risasi iliyofumua kichwa. Hiyo ilikuwa Julai 19, 1898.

Ni Mtaki ndiye aliyemtambua Mkwawa na kuwathibitishia Wajerumani kuwa ndiye mwenyewe. Wajerumani walimkata kichwa na fuvu lake kwenda kuliweka kwenye makumbusho ya Ubersee, Bremen, Ujerumani, kabla ya Julai 9, 1954, kurejesha fuvu hilo la Mkwawa na kuhifadhiwa kwenye Jumba la Makumbusho la Mkwawa, Kalenga, Iringa.

Baada ya Mkwawa kuuawa, Wajerumani hawakutimiza ahadi ya kumpa Mtaki uchifu wa himaya yote ya Wahehe. Waliamini kuwa kama aliweza kumsaliti Mkwawa, basi angeweza kuwasiliti Wajerumani wakati mwingine kama angeshawishiwa.

Himaya ya Wahehe ikagawanywa mara nne, ili wawe viongozi wenye himaya ndogondogo na kufanya kazi kwa muongozo wa Wajerumani. Uhehe Kati, kiongozi wake alikuwa Lusinde Mwang’ingo, Kaskazini-Magharibi, alipewa Msengidunda Mwamgongolwa, Kaskazini-Mashariki, Msatima Mwakindole na Kusini alisimikwa Mtaki.

MSALITI NI ASALI

Unachopaswa kuchukua ni hiki, kwamba msaliti ni asali kwa maana mara nyingi huwa ni mtu anayependwa na kuaminiwa. Tendo lake ni shubiri kwa sababu usaliti wake humuumiza mno aliyesalitiwa, kwani anakuwa hamtarajii kwa namna anavyomwamini.

Usaliti ukitendewa na mtu usiyemwamini wala humpendi wala siyo usaliti, ni matokeo tu na hayaumi. Usiyempenda na usiyemwamini humtarajii kwa lolote jema. Usaliti huuma kwa sababu huitwa usaliti kutokana na mguso wa mtenda usaliti kwa msalitiwa.

Wenye kuaminiwa na kupendwa hujifahamu kuwa wao ni asali ya wale wanaowapenda. Wakifahamu hayo yote huamua kufanya kitendo cha usaliti ambao ni tendo sawa na shubiri kwa aliyependa na kuamini.

Ukipendwa pendeka na uutunze huo upendo. Ukiaminiwa aminika na ulinde hiyo imani. Ukifanya hivyo utabaki kuwa asali ya anayekuamini na anayekupenda. Bila shaka unafahamu asali ilivyo tamu. Ukikengeuka na kumsaliti, hapohapo unageuka shubiri. Unajua mwenyewe shubiri ilivyo chungu.

Usishangae uadui mkubwa ambao hutokea kwa watu waliopendana lakini baadaye kutokea hata kuapizana kutoana roho. Ni kwa sababu tayari ile asali yote inakuwa imebadilika na kuwa shubiri. Asali ni upendo, unafahamu jinsi upendo ulivyo mtamu. Shubiri ni chuki, unajua namna chuki ilivyo chungu.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top