Sakata la kutoweka kwa kiongozi wa Chama cha demokrasia na maendeleo chadema, BEN SAANANE limechukua sura mpya baada ya chama hicho kutoa tamko rasmi kwamba hawajui alipo msaidizi huyo wa mwenyekiti wa taifa .
Akitoa tamko lao mwanasheria mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo chadema Tundu Lissu wameiomba serikali kupitia jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya mahali alipo BEN SAANANE, msaidizi wa mwenyekiti wa taifa upande wa siasa na jamii anayedaiwa kutoweka tangu novemba 14 mwaka huu na mara ya mwisho kupata taarifa zake inadaiwa aliwasiliana na mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.
Tundu Lissu amesema serikali ndio yenye ulinzi na udhibiti mkubwa wa mipaka ya nchi ambapo inao uwezo wa kufahamu kama mtu ametoka nje ya nchi au yupo ndani ya nchi hivyo amedai kuwa wanawajibu wa kufanya kila njia ya kumpata Ben Saanane ambaye taarifa za kutoweka kwake kwa mara ya kwanza zilitolewa na ndugu zake wa karibu.
Katika hatua nyingine CHADEMA pia imetaka uchunguzi wa kutosha juu ya maiti za watu zilizookotwa mto Ruvu ili kujiridhisha aina ya kifo chao licha ya kwamba taarifa za awali zilidai watu hao ni wahamiaji haramu.
Post a Comment