Tahadhari kuhusu manunuzi na matumizi ya Antivirus katika kifaa chako cha teknolojia.
Na Adimu Nihuka Jr.
Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama vile kompyuta, vinahitaji ulinzi mkubwa ili vifanye kazi kwa ufanisi.
Njia mojawapo ya kulinda vifaa vyako ni kutumia programu maalumu zinazojulikana kwa kitaalamu kwa jina la antivirus.
Hata hivyo, unapaswa kujua mambo kadhaa unapochagua programu nzuri itakayohakikisha usalama wa kifaa na wewe mwenyewe kwa asilimia kubwa.
Siku hizi antivirus haziingizwi kwenye kompyuta hasa zile za Windows. Zinaingizwa hata kwenye Mac na kwenye baadhi ya simu za kisasa na vifaa vingine vya mawasiliano .
Antivirus zinaweza kununuliwa kwa njia mbalimbali, lakini maarufu zaidi ni ile ya kununua CD dukani.
Kwa wenye kadi za malipo, wanapendelea zaidi kununua leseni tu kisha wanapewa kiunganishi cha kupakua ili waingize wenyewe.
Kama umenunua kwa njia ya mtandao, hakikisha tovuti uliyonunulia siyo batili maana kuna wengi wamelizwa kwa mtindo huu. Kama ni rafiki yako amekuletea kwa njia ya flash hakikisha ni safi. Ili kuepuka yote hayo, njia nzuri na bora zaidi ni kupata CD.
Kuna tofauti kubwa kati ya kuingiza antivirus mpya na kuboresha iliyopo (upgrade). Nakushauri kama antivirus yako imeisha muda wake, toa na weka toleo jipya. Unapo ‘upgrade’ unaweza kusababisha matatizo kwenye kifaa chako.
Angalia uwezo wa kompyuta yako kwenye vitu kama RAM na CPU, jiulize je, antivirus unayotaka kuweka itakubali? Pia utaangalia kwenye antivirus kwamba inaweza kuingizwa kwenye kompyuta yenye RAM na CPU.
Angalia antivirus yako kama inaingia kwenye Windows, Mac au aina nyingine ya Operating system, kwani siyo antivirus zote zinazoweza kuingia popote. Kwa kawaida kuna matoleo ya aina tatu ya antivirus; kuna yale ya bure, ya majaribio kwa siku 30 au 15 na matoleo ya kuuzwa yenye siku 365 sawa na mwaka mmoja .
Tofauti kati ya matokeo hayo ni kwamba yale ya bure unapewa kila kitu, lakini kuna baadhi ya vitu unaweza kukosa.
Hizi za majaribio unapewa kuitumia kwa siku kadhaa kabla ya wewe kuamua kununua au ijifunge yenyewe. Hata hivyo, kama unataka kujaribu bora utumie ile ya bure.
Baadhi ya kompyuta zenye Windows 8 na 10 huwa na antivirus zake moja kwa moja (windows Defender). Windows Defender ni nzuri, lakini haiwezi kukulinda na matatizo mengi yaliyopo kwa njia ya mtandao.Wahalifu wengi wana mbinu nyingi za kuizidi Windows Defender. Pia, kama umezoea aina fulani ya Antivirus kama ni Kaspersky au Symantec unashauriwa kuendelea kutumia hiyo hiyo kama haikuletei shida yoyote kulingana na matumizi yako. Kuhamia bidhaa nyingine, kuna gharama zake.
Vitu vingine unavyotakiwa kuangalia ni kama antivirus hiyo inaweza kufanya kazi na programu nyingine zote zilizopo katika kifaa chako.
Hapa naongelea programu zenye leseni halali, kama ni bandia ujue kuna shida mbalimbali zitatokea ikiwamo kufuta leseni zenyewe au mafaili ya programu.
Kumbuka antivirus haiwezi kuhakikisha usalama wa kifaa chako kwa asilimia 100 kama wewe mwenyewe hufuati taratibu za matumizi salama ya kifaa chako.
Kwa ushauri na miongozo zaidi, tafadhali wasiliana na fundi wa kompyuta wa ofisini kwako au hapo utakapokwenda kununua bidhaa. Lakini, muhimu zaidi uwe unasoma maelezo yote na kuelewa kabla ya kuamua kununua bidhaa yoyote
Post a Comment