DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Uamuzi wa Trump Waendelea kuleta maafa na matata
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
Mapambano baina ya wanajeshi wa usalama wa Israel na vijana wa Kipalestina yamechukua roho nyingi za wananchi. Vijana wa Kipalestina wanaru...


Mapambano baina ya wanajeshi wa usalama wa Israel na vijana wa Kipalestina yamechukua roho nyingi za wananchi. Vijana wa Kipalestina wanarusha mawe kuwashambulia wanajeshi wa Israel, lakini mara nyingi hujibiwa kwa risasi za moto. Mambo yamezidi tangu wiki mbili zilizopita pale Rais Donald Trump wa Marekani alipotangaza kwamba Serikali ya nchi yake inautambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa dola ya Israel na kwamba ubalozi wa Marekani utahamia Jerusalem kutokea Tel Aviv ulioko hivi sasa.

Uamuzi huo umewakasirisha Wapalestina, Waarabu na sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa. Katika azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nchi nyingi za Umoja huo ziliilaumu Marekani kwa kuchukua uamuzi huo na nchi zote duniani zimetakiwa zisiutambue mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Pia wasipeleke balozi zao katika mji huo.

Vijana wa Wapalestina wanahisi wamehadaiwa kuhusu mustakabali wao, na hasira zao zinaelekezwa katika kuwarushia mawe wanajeshi wa Israeli kila pale wanapopata nafasi. Kwa vijana hao suala si tu juu ya kuwa na dola ya Kipalestina iliyo na mji wake mkuu Jerusalem ya Mashariki, lakini kuwa na tamaa ya kupata ajira na kuishi bila ya woga.

Katika Jerusalem Mashariki na kwenye maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, pia kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza, vijana wa Kipalestina wameonyesha namna walivyovunjika moyo na wanatoa jasho lao kupinga uvamizi wa Waisraeli. Vitendo vya wanajeshi wa Israel kuwasaka na kuchunguza nyendo za vijana hao barabarani limekuwa ni jambo la kawaida.

Vizuizi vya njiani na mipakani vinawasumbua sana Wapalestina katika maisha yao ya kila siku. Vita vidogo vinaendeshwa na vijana wa Kipalastina waliofunika nyuso zao dhidi ya wanajeshi wa Tel Aviv.

Wengi wa vijana wanaoshiriki katika malalamiko wanahisi wameachwa katika mataa, hawaungwi mkono waziwazi na viongozi wa Kipalestina na pia hata na Dunia ya Kiarabu iliyobaki.

Mara mbili katika mikutano ya kilele ya nchi za Kiarabu Wapalestina walitaka Jerusalem Mashariki itambuliwe kuwa ni mji mkuu wa Wapalestina, lakini jambo hilo halijawekewa uzito wa kweli. Pia Wapalestina wamevunjika moyo na nchi za Ulaya, kwani nchi hizo hazijapendekeza mpango ulio wazi na madhubuti katika kuutatua mzozo wa Mashariki ya kati.

Umoja wa Ulaya haujataka kuwa mezani mipango ya kukabiliana na Marekani kuhusu suala la mzozo baina ya Wapalestina na Israel.

Hali hizo zote za kuvunjika moyo zimezidi tangu pale Rais Donald Trump alipotoa lile tangazo lake la Desemba 6, na baadaye mambo yakapamba moto. Bila ya kuungwa mkono na kusaidiwa, bila ya kuwa na matarajio, vijana wa Kipalestina yaonyesha wameishiwa kabisa na subira. Walichobakia kutumia dhidi ya wanajeshi wa Israel, kwa masikitiko, ni mawe na visu.

Mara nyingi vijana hao wakati huo huo hukabiliwa na Waisraeli ambao nao pia huwa na woga na hujibu hujuma za kurushiwa mawe kwa nguvu za kupita kiasi. Hata hivyo, mtu yeyote aliyewahi kupigwa jiwe anatambua kwamba jambo hilo linaweza kuwa ni shambulio dogo lakini si la kulidharau. Lakini ilikuwaje wanajeshi wa Kiisraeli wakawaua kwa risasi Wapalestina wawili ambao walikuwa upande wa pili wa mpaka katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa?

Baadaye ilijulikana kwamba Wapalestina hao waliouliwa hawajawa na silaha. Yaonyesha kila pale mapambano yanapozidi ndipo watu wanapofyatuliwa risasi za moto. Kitendo cha baadaye ambapo alipigwa risasi Mpalestina ambaye yaonesha alimjeruhi kwa kisu polisi wa mpakani na alivaa mkanda uliojaa baruti, kinaweza kutathminiwa kuwa ni kitendo cha kujilinda.

Tangu Trump alipotoa tangazo lake, watu wanaoishi upande wa Israel kuzunguka Ukanda wa Gaza kila siku husikia sauti kali za ving’ora. Si chini ya maroketi 14 yalifyatuliwa katika siku zilizopita kutokea Ukanda wa Gaza kwenda maeneo ya Israel. Roketi moja liliupiga mji wa Sderot ulio na wakazi 20,000. Bahati nzuri ilikuwa ni jioni na si watu wengi walikuwa nje ya nyumba zao. Magari na shule ya chekechea yaliathirika. Mengi ya maroketi hayo yalizuiliwa hewani na mfumo wa kujikinga wa Israel.

Watu wanane wamekufa na zaidi ya mia moja wamejeruhiwa. Hayo ndiyo matokeo ya tangazo la Trump la kutaka kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem na kuutambua mji huo kuwa mji mkuu wa Israel. Lakini sasa pia Israel inahisi imevunjwa moyo na Marekani. Ilitarajia kwamba tangazo la Trump litatekelezwa mara moja. Kumbe sivyo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Rex Tillerson ametangaza: Ubalozi wa Marekani mapema sana utahamishiwa Jerusalem mwaka 2020 au baada ya mwisho wa kipindi cha sasa cha Rais Trump.

Machafuko ya karibuni baina ya vijana wa Kipalestina na wanajeshi wa Israel yalisheheni hasa katika Jerusalem, Ramallah, Hebron na Bethlehem, pia katika Ukanda wa Gaza. Huko Bethlehem na Nazareth mapambano, kama ilivyo kawaida, yalikuwa sehemu ya matayarisho kabla ya sherehe za Krismasi. Mamia ya wanajeshi na polisi wa mipakani walitumwa upande wa Gaza na kwenye maeneo yaliyoko Magharibi ya Mto Jordan. Wapalestina kadhaa walikamatwa. Katika Ukingo wa Magharibi idadi kubwa ya watu katika historia ya karibuni walikamatwa, 421 katika Jerusalem na karibu ya 80 katika Jerusalem ya Mashariki. Hao waliokamatwa walituhumiwa kuendesha harakati za kigaidi na kuchafua nidhamu na sheria.

Meya wa Nazareth, Ali Salam alitangaza kusimamishwa baadhi ya shughuli za Krismasi, kulikuwa hakuna nyimbo na watu kujitokeza katika majukwaa ya hadharani. “Uamuzi wa Trump umetunyima furaha,” alisema meya huyo juu ya hatua hiyo. Nazareth ni mahala ambapo Malaika Gabriel alimuarifu Maria juu ya kuzaliwa Yesu. Kwa mujibu wa Biblia ni kwamba Yesu alikulia Nazareth na ndiyo maana watalii wengi huutembelea mji huo, hasa wakati wa Krismasi. Wengi wa wakazi wake 75,000 – theluthi moja ni Wakristo na theluthi mbili ni Waislamu – wanategemea maisha yao kwa biashara ya utalii.

Ilipofika Desemba 21, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York lilipiga kura kuitaka Marekani iachane na uamuzi wake wa kuitambua Jerusaelm kama mji mkuu wa Israel, licha ya Rais Trump kutishia hapo kabla kwamba zile nchi zitakazokubaliana na azimio juu ya Jerusalem zitaadhibiwa kwa kunyimwa misaada ya Marekani. Nyingi ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilikubaliana na azimio hilo ambalo lilielezea masikitiko makubwa juu ya uamuzi wa Marekani.

Nchi 128 kati ya 193 katika Umoja wa Mataifa zililiunga mkono azimio hilo, ikiwemo Tanzania, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na hata Austria. Nchi 35 zilijizuia kupiga kura, ikiwemo Kenya, na tisa zilipinga, zikiwemo Marekani, Togo na Guatemala. Azimio hilo si lenye kuzilazimisha nchi kulitekeleza, kwa hivyo athari zake ni kama alama tu. Linaonesha kwamba jamii ya kimataifa si tu inaunga mkono haki ya Wapalastina na kwamba Jerusaelm ni mji mkuu wa baadaye wa dola ya Palestina, lakini pia ni kwamba linaheshimu sheria ya kimataifa na linaikataa siasa ya nchi kuzibinya nchi nyingine.

Nchi zilizoliunga mkono azimio hilo zimedhihirisha kwamba hazitetereki na vitisho au uwezekano wa kunyimwa misaada, lakini kwao haki na sheria za kimataifa ndiyo mwongozo wa siasa zao za kigeni. Ni kufuata siasa hiyo tu ndipo dunia yetu hii inaweza kubakia salama, licha ya changamoto nyingi na kubwakubwa zilioko mbele yetu sisi wanadamu. Ubabe wa Marekani umepigwa kofi tena mara hii. Je, hilo ni somo kwa Donald Trump?

Chanzo Mwananchi

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top