DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Bunduki 37 zakamatwa na polisi Tanga
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
Bunduki 37 zakamatwa JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limekamata silaha za aina mbalimbali zikiwemo bunduki 37, wakati wa operesheni maalumu ...

Bunduki 37 zakamatwa

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limekamata silaha za aina mbalimbali zikiwemo bunduki 37, wakati wa operesheni maalumu zilizofanywa kwa nyakati tofauti na askari mwaka huu, kwa lengo la kupambana na kudhibiti matukio ya uhalifu na unyang'aji wa kutumia silaha.

Bunduki hizo zilikamatwa zikiwa pamoja na risasi 474 ambapo 425 kati ya hizo zilikuwa za aina ya SMG, 24 za shotgun na 25 zilikuwa za rifle.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Benedict Wakulyamba ametoa taarifa hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kuzungumzia hali ya usalama na kusema takwimu hizo zimekusanywa kuanzia Januari hadi Novemba 2016.

"Tulikamata bunduki aina ya SMG nane, Marker IV mbili, shotgun nne, bastola moja, gobori 20, rifle mbili ambazo zilipatikana kwenye matukio mbalimbali ya uhalifu pamoja na mabomu manne ya kurushwa kwa mkono," alisema.

Kamanda Wakulyamba katika taarifa yake hiyo alisema mwaka huu idadi ya kesi zilizofunguliwa kutokana na matukio ya uhalifu zimepungua kutoka 21,166 za mwaka 2015, hadi kufikia kesi 20,601 mwaka huu.

"Mwaka huu kuna upungufu wa kesi 565 sawa na asilimia 2.67 ikilinganishwa na za mwaka uliopita ambapo jumla ya kesi 7,056 kati ya zote zilizofunguliwa ziliweza kifikishwa mahakamani. Kesi 2,198 kati ya hizo, washtakiwa walitiwa hatiani na kupewa adhabu mbalimbali ambapo kesi nyingine 1,472 washtakiwa wake mahakama iliamua kuwaachia huru kwa mujibu wa sheria," alisema.

Aidha, alisema kesi nyingine 9,875 ziko katika hatua mbalimbali za uendeshaji mahakamani ambapo baadhi zinaendelea kupelelezwa.

Akizungumzia udhibiti wa dawa za kulevya, kamanda huyo alisema kesi 294 zinazohusisha ukamataji wa kilo 1,188.2 za bangi kwa nyakati tofauti zilifunguliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi. "Dawa za kulevya aina ya mirungi zilifunguliwa kesi 165 baada ya kukamatwa kilo 2,268.3.

Kwa upande wa dawa za kulevya ambazo zinatumika katika shughuli za uzalishaji viwandani tulifungua kesi 54 zilizohusisha kukamatwa kwa gramu 130.48 za aina tofauti za dawa hizo," alisema.

Akizungumzia uingiaji wa wahamiaji haramu hapa nchini kwa kupitia maeneo ya mkoa wa Tanga, alisema katika kipindi hicho walikamatwa wahamiaji 168 kutoka Ethiopia, 73 Somalia, 10 kutoka Kenya ambapo wahamiaji hao waliweza kukabidhiwa kwenye taasisi husika kwa hatua zaidi za kisheria.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top