DobsFoundation  DobsFoundation Author
Title: Mashamba 193 hatarini kufutwa
Author: DobsFoundation
Rating 5 of 5 Des:
SERIKALI wilayani Kilosa, Morogoro imefanya uhakiki na kubaini kuwa mashamba pori yapo 193 yenye jumla ya hekta 262,648 sawa na ekari 656,6...

SERIKALI wilayani Kilosa, Morogoro imefanya uhakiki na kubaini kuwa mashamba pori yapo 193 yenye jumla ya hekta 262,648 sawa na ekari 656,621, imeelezwa. Mashamba mengi kati ya hayo yanakadiriwa yalipimwa tangu miaka ya 1930, kipindi ambacho wakazi wa wilaya ya Kilosa walikuwa wachache.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, alisema hayo juzi kupitia taarifa yake ya shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo kwa Mkuu wa mkoa, Dk Kebwe Stephen.

Hata hivyo, alisema katika uhakiki huo ilibainika mashamba yenye ukubwa wa jumla ya hekta 536,590 yenye hati miliki ambayo yanamilikiwa na wawekezaji yanafaa kwa kilimo.

Mgoyi alitaja idadi ya mashamba yaliyokaguliwa kuwa ni 74, ambapo mashamba manne yamebainika wamiliki wake walikopa fedha benki, sita yalitaifishwa, mashamba manne yalibatilishwa na mashamba 17 yaliombewa kibali cha kufutwa.

Alisema, "kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya ina wakazi 438,175 na kwa ongezeko la mwaka 2016 inakadiriwa kufikia idadi ya watu wapatao 485,375 na asilimia 88 ya wananchi hao ajira yao kubwa ipo kwenye kilimo," alisema.

Hivyo alitaja orodha ya mashamba yaliyobatilishwa, mmiliki wake na ukubwa wake ni Magole Farms Enterprises lenye ukubwa wa ekari 525 lililopo Magole, M/S Agro Industries Ltd ukubwa wa ekari 1,008 katika eneo la Msowero.

Shamba lingine ni la M/S Agro Industries Ltd ekari 1,384, pia eneo la Msowero pamoja na la Islam Mohammed Nahdi & Mohamed Nahdi lililopo eneo la Manyenyere, Kimamba. Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, mashamba yaliyoombewa mkopo benki ni M/S New Kimamba Fibres Co Ltd yenye namba 342, ukubwa wa ekari 7,367 lililopo Kimamba na sehemu kubwa ya shamba linalimwa mkonge.

Alitaja shamba lingine ni la Ameir Mbarak lenye namba 119 likiwa na ukubwa wa ekari 388 eneo la Myombo amblo linalimwa kwa kuwakodishia wananchi na halijalipiwa kodi toka mwaka 2013 na mmiliki ameliwekea dhamana benki.

Mkuu wa wilaya huyo katika taarifa yake kwa mkuu wa mkoa, alitaja shamba lingine ni la M/S Sumagro Ltd yenye namba 121 na ukubwa wa ekari 7,712 lililopo eneo la Madoto ambapo ekari 100 zimelimwa mkonge, sehemu uliyobaki ni pori na mmiliki wake amelikopea benki tangu mwaka 2003.

Mgoyi pia alitaja shamba lingine ni la Sadrudin K.V, Amirali A.M.B Badrudina A.B na Nurdin L.M lenye namba 38 na ukubwa wa ekari 476 lilipo eneo la Magole ambalo linakaliwa na wananchi wa Magole kwa makazi na shughuli za kilimo na inaonesha mmiliki wake amelikopea benki tangu mwaka 2004.

Mashamba mengine ambayo serikali iliyataifisha mwaka 1974 ni M/S Twika Diary lenye ukubwa wa ekari ,3,120 na jingine la mmiliki huyo lenye ukubwa wa ekari 3,690 yakiwa kaika eneo la Mbwade.

Shamba lingine ni M/S Mbugani Sisal Estate lenye ukubwa wa ekari 2,840 lililopo Madulu, shamba la M/S Ulaya Sisal Estate lenye ukubwa wa ekari 3,990 lililopo Kata ya Ulanga, licha ya shamba hilo kukabidhiwa halmashauri ya wilaya ya Kilosa miaka ya 1980, hati zake zimewekwa reheni benki na wamiliki wa mwanzo.

Pia katika taarifa yake, aliyataja mashamba mengine matatu tofauti yenye ekari 564, 546 na 488 ya mmiliki Sadjudin Rajabali Meghji yaliyotaifishwa mwaka 1974 yamevamiwa na wananchi wanalima mazao mbalimbali ya msimu na ya kudumu.

Hata hivyo alisema kwa sasa kuna kesi ya Rufaa namba 227 ya mwaka 2008 mahakama kuu kitengo cha ardhi baina ya mmiliki wa awali na wanaodaiwa kuvamia.

Mkuu wa Mkoa Dk Kebwe, aliuangiza uongozi wa wilaya kuwasilisha orodha yakinifu ya mashamba pori yote na kuviagiza vyombo vya dola wilayani humo kuwakamata madalali wanaoendesha biashara ya kukodisha mashamba na kujipatia fedha.

"Madalali wa kukodisha mashamba wamekuwa na tabia ya kuwaita watu kutoka mikoa ya nje na wa ndani, wakamatwe tayari orodha ya majina yao tunayo , kwa kuwa wanatuletea migogoro baina ya wakulima na wafugaji," alisema.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top